Friday, July 10, 2015

KIFO WAJAMANI KIFO!

Kifo chamtwaa hima, mwenye rembo harembui,
Mwenye hadhi alo wima, na wala hajawa mui,
Mwenye hazui tuhuma, na wenza hawashitui,
Mgamba hakichagui, kinatupokonya mwema!

Huiba mwenye hekima, mwenye ni finyu hajui,
Mwenye yakwe taaluma, hiyau hawasumbui,
Mwenye kushauri umma, kwa mambo ya kila nui,
Mngamba hakichagui, chamkimbilia mwema!

Huwinda mwenye huruma, mwenye mwanzo habeui,
Mzuri wa taadhima, mwenye chache maadui,
Unyo kinamuandama, akafa hatufufui,
Mngamba hakichagui, chamkimbilia mwema!

Huvuna mwenye kuvuma, mwenye sambi hazuzui,
Mwenye mbee kusukuma, wale hawajitambui,
Mwenye hana uhasama, kadhalika habagui,
Mngamba hakichagui, chamkimbilia mwema!

Humchukua mapema, augue haugui,
Hoyo upesi huhama, tubaki hatuzumbui,
Pengo aliache nyuma, itukie hatukui,
Mngamba hakichagui, chamkimbilia mwema!

(roho yake mwendazake Ustadh Omar Babu “Abu Marjan” na ilazwe pema peponi)

Twitter: @RedscarMcOdindo

No comments:

Post a Comment